Psalms 69

Kilio Cha Kuomba Msaada Wakati Wa Dhiki

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yungiyungi. Zaburi ya Daudi)


1 aEe Mungu, niokoe,
kwa maana maji yamenifika shingoni.

2 bNinazama kwenye vilindi vya matope,
pasipo mahali pa kukanyaga,
Nimefika kwenye maji makuu,
mafuriko yamenigharikisha.

3 cNimechoka kwa kuomba msaada,
koo langu limekauka.
Macho yangu yanafifia,
nikimtafuta Mungu wangu.

4 dWale wanaonichukia bila sababu
ni wengi kuliko nywele za kichwa changu;
wengi ni adui kwangu bila sababu,
wale wanaotafuta kuniangamiza.
Ninalazimishwa kurudisha
kitu ambacho sikuiba.


5 eEe Mungu, wewe unajua upumbavu wangu,
wala hatia yangu haikufichika kwako.


6 Ee Bwana, ewe Bwana Mwenye Nguvu Zote,
wakutumainio wasiaibishwe
kwa ajili yangu;
wakutafutao wasifedheheshwe kwa ajili yangu,
Ee Mungu wa Israeli.

7 fKwa maana nimestahimili dharau kwa ajili yako,
aibu imefunika uso wangu.

8 gNimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,
mgeni kwa wana wa mama yangu mwenyewe.

9 hKwa kuwa wivu wa nyumba yako unanila,
matukano ya wale wanaokutukana yameniangukia.

10 iNinapolia na kufunga,
lazima nivumilie matusi.

11 jNinapovaa nguo ya gunia,
watu hunidharau.

12 kWale wanaoketi mlangoni wananisimanga,
nimekuwa wimbo wa walevi.


13 lLakini Ee Bwana, ninakuomba,
kwa wakati ukupendezao;
katika upendo wako mkuu, Ee Mungu,
unijibu kwa wokovu wako wa hakika.

14 mUniokoe katika matope,
usiniache nizame;
niokoe na hao wanichukiao,
kutoka kwenye vilindi vya maji.

15 n oUsiache mafuriko yanigharikishe
au vilindi vinimeze,
au shimo lifumbe kinywa chake juu yangu.

16 pEe Bwana, unijibu, kwa wema wa upendo wako;
kwa huruma zako nyingi unigeukie.

17 qUsimfiche mtumishi wako uso wako,
uharakishe kunijibu, kwa sababu niko katika shida.

18 rNjoo karibu uniokoe,
nikomboe kwa sababu ya adui zangu.


19 sUnajua jinsi ninavyodharauliwa,
kufedheheshwa na kuaibishwa,
adui zangu wote unawajua.

20 tDharau zimenivunja moyo
na nimekata tamaa,
nimetafuta wa kunihurumia, lakini sikumpata,
wa kunituliza, lakini sikumpata.

21 uWaliweka nyongo katika chakula changu
na walinipa siki nilipokuwa na kiu.


22 vMeza iliyoandaliwa mbele yao na iwe mtego,
nayo iwe upatilizo na tanzi.

23 wMacho yao yatiwe giza ili wasiweze kuona,
nayo migongo yao iinamishwe daima.

24 xUwamwagie ghadhabu yako,
hasira yako kali na iwapate.

25 yMahali pao na pawe ukiwa,
wala asiwepo yeyote atakayeishi katika mahema yao.

26 zKwa kuwa wanawatesa wale uliowajeruhi,
na kuzungumza juu ya maumivu ya wale uliowaumiza.

27 aaWalipize uovu juu ya uovu,
usiwaache washiriki katika wokovu wako.

28 abWafutwe kutoka kitabu cha uzima
na wasiorodheshwe pamoja na wenye haki.


29 acMimi niko katika maumivu na dhiki;
Ee Mungu, wokovu wako na unihifadhi.


30 adNitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,
nami nitamtukuza kwa kumtolea shukrani.

31 aeHili litampendeza Bwana kuliko ng’ombe dume,
zaidi ya fahali akiwa na pembe na kwato zake.

32 afMaskini wataona na kufurahi:
ninyi mnaomtafuta Mungu, mioyo yenu na iishi!

33 ag Bwana huwasikia wahitaji
wala hadharau watu wake waliotekwa.


34 ahMbingu na dunia zimsifu,
bahari na vyote viendavyo ndani yake,

35 aikwa maana Mungu ataiokoa Sayuni
na kuijenga tena miji ya Yuda.
Kisha watu watafanya makao yao humo na kuimiliki,

36 ajwatoto wa watumishi wake watairithi
na wale wote walipendao jina lake
wataishi humo.
Copyright information for SwhKC